Jinsi ya kupiga picha vipengele vya ufikiaji

Picha dhahiri zilizo na maelezo mafupi husaidia wageni kuamua iwapo eneo lako linakidhi mahitaji yao.
Na Airbnb tarehe 22 Sep 2020
video ya dakika 4
Imesasishwa tarehe 2 Des 2024

Wageni wanataka kujua kwamba wataweza kusogea kwa usalama na starehe katika nyumba kabla ya kuweka nafasi. Kushiriki picha dhahiri na za kina za vipengele vya ufikiaji huwasaidia wageni kuamua ikiwa nyumba yako inakidhi mahitaji yao mahususi.

"Ninaweza kujua kutoka kwenye picha moja ikiwa sehemu itanifaa," anasema George, mgeni anayetumia kiti cha magurudumu. “Au ‘Samahani watu, mnaweza kuisogeza meza hiyo?’ Kisha hiyo ni sawa kabisa.”

Airbnb hutathmini vipengele vyote vya ufikiaji na picha kabla ya kuonekana katika sehemu ya Vipengele vya ufikiaji kwenye tangazo, ambayo ni tofauti na matunzio ya picha au ziara ya picha.

Miongozo ya jumla

Fuata miongozo hii ili uweke vipengele vya ufikiaji kwenye tangazo lako. Ikiwa picha haikidhi vigezo fulani, tunaweza kukuomba upakie picha tofauti au uondoe kipengele hicho kwenye tangazo lako.

  • Toa angalau picha moja ya kila kipengele cha ufikiaji katika nyumba yako.
  • Weka utepe wa kupimia kwenye picha ili kuonyesha vipimo, kama vile upana wa mwimo wa mlango na kimo cha kaunta.
  • Pakia picha kadhaa za kila kipengele kutoka kwenye mitazamo tofauti ili kuwasaidia wageni kuelewa vizuri chumba au sehemu.
  • Andika maelezo mafupi yanayosaidia kufafanua vipengele vya ufikiaji vya vyumba na sehemu za wazi, kama vile maelezo kuhusu mwangaza.
  • Wajulishe wageni ikiwa ni maeneo fulani tu yanayofikika. Kwa mfano, "Hili ndilo bafu pekee katika nyumba lililo na ufikiaji usio na ngazi, mlango mpana na vyuma vya kujishikilia."

Vidokezi vya kupiga picha

Jaribu vidokezi hivi vya kupiga picha vipengele vya ufikiaji vya nyumba yako.

Ufikiaji usio na ngazi wa kuelekea kwenye nyumba

Onyesha kwamba hakuna ngazi au vizuizi vinavyozidi inchi 2 (sentimita 5) kwenye mlango wa nyumba au kwenye kijia kinachoelekea kwenye nyumba hiyo. Hii inajumuisha vijia vya kutembelea kando ya barabara vya nje, ushoroba, lifti na vipengele vingine ambavyo wageni lazima watumie kuingia ndani.

  • Fungua milango na malango yote kwenye kijia kinachoelekea mlangoni mwa nyumba. Ikiwa ufikiaji hauna ngazi na una vidato vinavyobebeka au vya vizingiti, hakikisha vipo.
  • Anzia mahali ambapo wageni wanawasili au kuegesha, ukipiga picha kila baada ya futi 10 (mita 3) kwenye kijia kinachoelekea mlangoni. Inamisha kamera kidogo kuelekea ardhini ili upige picha sehemu ya juu ya njia hiyo.
  • Piga picha tofauti ya mlango ukiwa nje. Rudi nyuma angalau futi 8 (mita 2.4) ili upige picha mlango ulio wazi, ukionyesha kijia kwenye pande zote mbili za kizingiti.

Ufikiaji usio na ngazi wa kuelekea chumbani

Onyesha vyumba na sehemu ambazo zinaweza kufikiwa bila ngazi, viungo au vizingiti vinavyozidi inchi 2 (sentimita 5). Piga picha sehemu za ndani na nje, ikiwemo sitaha, roshani na baraza zozote.

  • Fungua mlango kabisa ili upige picha ya karibu ya kizingiti. Inamisha kamera kidogo kuelekea sakafuni ili upige picha kijia kwenye pande zote mbili za sakafu au kiungo.
  • Rudi nyuma angalau futi 5 (mita 1.5) ili upige picha ufikiaji wa chumba ukiwa nje.
  • Rudia hatua hii na upige picha sawa ukiwa ndani ya chumba.
  • Ikiwa chumba kina sehemu kadhaa za kuingia, piga picha kila moja.
  • Piga picha za ziada ili kuonyesha kijia kinachoelekea kwenye mlango mkuu unaoingia kwenye chumba hicho.

Milango mipana ya kuingia

Onyesha milango kwenye nyumba yako ambayo ina upana wa angalau inchi 32 (sentimita 81). Kujua upana halisi wa mlango wa mbele na sehemu nyingine za kuingia huwasaidia wageni kuamua iwapo sehemu inaweza kukidhi kiti chao cha magurudumu au kifaa cha kutembea.

  • Fungua mlango kwa upana kadiri iwezekanavyo. Panua utepe wa kupimia kwenye fremu nzima. Hakikisha kwamba ncha zote mbili za utepe wa kupimia na nambari zake zimeonyeshwa wazi.
  • Piga angalau picha mbili: moja ya mlango ulio na utepe wa kupimia kwenye fremu na moja ambayo ni picha ya karibu ya kipimo cha mwisho, ili iwe rahisi kusoma.

"Ikiwa tunajua vipimo vya mlango, najua ikiwa kiti changu kitatoshea vizuri," George anasema.

Marekebisho ya bafuni

Onyesha vipengele vinavyoweza kuwasaidia wageni kusogea bafuni, ikiwemo bafu lisilo na ngazi, choo na vyuma vya kujishikilia bafuni na bomba la mvua au kiti cha kuogea. Toa picha zinazoonyesha bafu zima na bomba la mvua, pamoja na mionekano ya karibu ya vipengele mahususi ulivyonavyo.

  • Bafu lisilo na ngazi: Fungua pazia au milango. Inamisha kamera kidogo kuelekea sakafuni ili kuonyesha kwamba hakuna vizingiti au vizuizi vyovyote vya maji vilivyo juu zaidi ya inchi 1 (sentimita 2.5).
  • Vyuma vya kujishikilia: Onyesha wazi mahali palipo vyuma vya kujishikilia bafuni na karibu na choo. Piga picha tofauti za kila moja, hata kama pia unavionyesha pamoja kwenye picha pana za bafuni.
  • Kiti cha kuogea: Onyesha kiti kizima ndani ya bafu au beseni la kuogea, iwe kimewekwa kwenye ukuta au kinajitegemea.

Maegesho ya walemavu

Onyesha sehemu yako binafsi ya maegesho kwa ajili ya gari moja ambalo lina upana wa angalau futi 11 (mita 3.35) au eneo la maegesho la umma ambalo limetengwa kwa ajili ya mtu mwenye ulemavu.

  • Maegesho ya binafsi: Piga picha ukiwa mbali, huku gari likiwa limeegeshwa karibu na sehemu ya mgeni kwa ajili ya marejeleo. Au tumia utepe wa kupimia ili kuthibitisha upana wa sehemu hiyo.
  • Maegesho ya umma: Piga picha ya ishara na alama nyingine za barabarani zinazoonyesha kwamba sehemu hiyo imetengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Kijia chenye mwangaza kinachoelekeza kwenye mlango wa mgeni

Onyesha kwamba kijia au kijia cha kutembelea kando ya barabara kinachoelekea kwenye mlango wa mgeni kina mwangaza wa kutosha wakati kuna giza.

  • Washa vyanzo vyote vya mwangaza wa nje vinavyoangazia njia.
  • Zima taa zozote za ndani zinazoingilia mwangaza wa nje.
  • Hakikisha picha zako zinaonyesha mahali taa za nje zilipo kuhusiana na kijia.

Vifaa vya kumwinua mtu

Onyesha vifaa vyovyote vyenye injini au vya mikono katika nyumba yako ambavyo vimeundwa mahususi ili kuwasaidia wageni kuingia na kutoka kwenye kiti cha magurudumu, bwawa la kuogelea au beseni la maji moto.

  • Piga picha kifaa cha kumwinua mtu ukionyesha maelezo ya kina kadiri iwezekanavyo, ikiwemo iwapo kinaning'inia darini au kinajitegemea.
  • Piga picha pana inayoonyesha wazi mahali kilipo kando ya kitanda, choo, bwawa la kuogelea au beseni la maji moto.
  • Piga picha eneo la karibu ili kuonyesha ukubwa na nafasi yake kinapotumika.

Pata maelezo zaidi kuhusu matakwa ya kuweka vipengele vya ufikiaji kwenye tangazo.

Taarifa zilizomo kwenye makala hii zinaweza kuwa zimebadilika tangu zilipochapishwa.

Airbnb
22 Sep 2020
Ilikuwa na manufaa?