Nenda mbele ili upate matokeo yaliyopendekezwa

  Kukabiliana na mgogoro wa Ukrainia kwa kutoa msaada wa haraka

  Mamilioni walikimbia vita. Maelfu ya Wenyeji wa Airbnb.org waliwakaribisha.
  Na Airbnb tarehe 19 Ago 2022
  video ya dakika 4
  Imesasishwa tarehe 25 Ago 2023

  Vidokezi

  • Katika miezi iliyofuatia uvamizi wa 2022, watu milioni 6 walikimbia Ukrainia wakitafuta usalama

  • Wenyeji walifungua nyumba zao ili kuisaidia Airbnb.org kutimiza ahadi ya kuwapa watu 100,000 makazi ya muda

  Katika wiki iliyofuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukrainia, mwigizaji na Mwenyeji Rafał aliweza kuhisi athari zake katika mji wake wa Wroclaw, kusini magharibi mwa nchi ya Polandi. Masanduku ya vifaa vilivyochangwa yalijaa nje ya kituo cha utamaduni cha Ukrainia katika kitongoji chake. Alisikia lugha ya Kiukrainia ikizungumzwa mitaani na madukani.

  Baada ya muda mfupi, familia tatu kutoka Ukrainia ziliweka nafasi ya sehemu za kukaa za mwezi mzima, kwa mfuatano, kwenye nyumba anayoitangaza kwenye Airbnb. Akiwa na wasiwasi kuhusu kuwatoza watu wanaokimbia vita, Rafał aliwasiliana na kitengo cha huduma kwa wateja cha Airbnb, akafahamu kwamba Airbnb.org inaweza kugharamia kwa sehemu juhudi zake na akajisajili.

  Kulingana na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 7 walikimbia Ukrainia katika miezi sita baada ya uvamizi wa mwezi Februari mwaka 2022. Mamilioni ya familia waliwasili katika majiji kote barani Ulaya wakiwa na masanduku machache tu na hawakujua hata kidogo lini watarudi nyumbani.

  Kwa kuitikia mgogoro huo, Airbnb.org ilitoa mwito kwa washirika wake wasiotengeneza faida na jumuiya ya kimataifa ya Wenyeji: Je, unaweza kutusaidia kutoa makazi ya muda kwa hadi watu 100,000 wanaokimbia Ukrainia?

  Tangu wakati huo, Airbnb.org imetimiza lengo hilo, kutokana na usaidizi mkubwa wa kimataifa kutoka kwa Wenyeji, wafadhili wa Airbnb.org na mashirika ya kibinadamu yanayowasaidia watu mashinani.

  Baadhi ya watu walioitikia mwito huo, kama vile Rafał, ni Wenyeji wa Airbnb wa muda mrefu ambao hutoa sehemu za kukaa kwa punguzo kupitia Airbnb.org katika wakati huu wa shida. Wengine, kama vile Mary, mwanasayansi wa takwimu wa Marekani anayeishi huko Berlin, walikuwa miongoni mwa Wenyeji wapya 40,000 ambao walijisajili ili kutoa sehemu za kukaa za bila malipo au zenye punguzo kupitia Airbnb.org kwa wageni wakimbizi.

  Airbnb.org ilinipa njia thabiti ya kuchukua hatua.
  Host Mary of Berlin

  Kutafuta njia ya haraka ya kusaidia

  Rafał, mwigizaji na Mwenyeji wa Airbnb, alijisajili kwenye Airbnb.org mara baada ya vita kuanza.

  Rafał anasema uvamizi wa Ukrainia ulimshtua kila mtu aliyemjua nchini Polandi, hata hivyo, alishangaa jinsi marafiki na majirani wake walivyoitikia kwa haraka mmiminiko wa watu waliokuwa wakikimbia vita. Watu walichangia chakula katika kituo cha treni cha Wroclaw na wakakusanya vifaa vya kupeleka kwenye mpaka wa Ukrainia.

  Alianza kuandaa onyesho la muziki la kuchangisha fedha na wenzake, lakini pia alitaka kutafuta njia ya haraka zaidi ya kusaidia. "Kukosa sehemu ya kukaa, mahali pa kulala, ni mojawapo ya hali mbaya zaidi," anasema.


  Rafał anaendelea kutangaza nyumba yake kupitia Airbnb.org ili kuwakaribisha wageni waliohamishwa na migogoro. Pia amesaidia kukalimani mafunzo ya Airbnb.org kupitia mtandao kwenda Kipolishi.

  Kutoa sehemu salama

  Katika kipindi cha miezi miwili mwaka 2022, Mary alikaribisha watu wanne waliokimbia Ukrainia.

  Huko Berlin, karibu maili 215 (kilomita 350) kaskazini magharibi mwa Wroclaw, Mary alifuatilia habari kuhusu uvamizi wa Ukrainia. Alipoona wito wa Airbnb.org wa kuchukua hatua mtandaoni, alitangaza fleti yake bila malipo.

  Mfanyakazi kutoka Shirika la Organization for Refuge, Asylum, and Migration (ORAM), shirika moja wapo kati ya washirika wa Airbnb.org, aliwasiliana naye. Kama ambavyo vyombo vingi vya habari vimeripoti, hisia dhidi ya LGBTQ+ nchini Ukrainia na baadhi ya nchi jirani zimeongeza hatari kwa watu wa LGBTQ+ waliohama makazi yao wakati wa mapigano haya. Mwakilishi huyo wa ORAM alimuuliza Mary iwapo watu wawili wenye utambulisho tofauti wa kijinsia wanaweza kukaa kwenye nyumba yake.

  Mary alifurahi kuwakaribisha wageni wa LGBTQ+. "Nilijua kwamba fleti yangu ilikuwa sehemu salama sana kwao," anasema.

  Kukuza muunganisho

  Mara baada ya wageni wa kwanza wa Mary kuondoka, Dima aliwasili ili kukaa kwa wiki mbili. Mwanamume shoga mwenye umri wa miaka 20 na kitu, Dima alikuwa akiishi huko Kyiv wakati Warusi walipoanza kulipua mabomu jiji hilo. Shirika la mashinani linaloitwa Safebow lilimsaidia Dima na paka wake, Peach, kusafiri kupitia nchini Polandi hadi jijini Berlin. Akiwa huko, ORAM ilimsaidia kupata makazi na kujisajili kwa huduma za kijamii.

  Baada ya safari iliyojaa vizuizi, Dima alifarijika alipowasili kwenye fleti ya Mary. "Nilikuwa na hisia nyingi sana siku hizo za kwanza," anasema. "Sijui hata ni jambo gani lililokuwa muhimu zaidi kwangu: kuwa katika sehemu salama au kuelewa tu kiasi cha usaidizi ambacho ninapokea."

  Mary alikuwa nje ya mji kwa wiki ya kwanza tangu Dima aanze kukaa kwake. Aliporudi Berlin, wawili hao waliingiana vizuri. Walikaa saa nyingi kwenye meza yake ya jikoni, wakila pamoja na kunywa bia. Waliendelea kuwasiliana baada ya Dima kuhamia kwenye fleti nyingine.

  "Kilikuwa kichocheo kikubwa kwa mwanzo wa maisha yangu hapa," Dima anasema.

  Kufanya tofauti

  Mary anaendelea kutafakari jinsi kukaribisha wageni kulivyoonekana kuwa rahisi. “Sikufanya jambo lolote la ajabu hasa,” anasisitiza. “Nilichukua nafasi. Labda nilipata usumbufu mdogo tu.”

  Anatofautisha hilo na masimulizi ambayo wageni wake wamesimulia: "Ninafikiria kuhusu kushughulika na [mambo] katika eneo geni kabisa, eneo ambalo sikuchagua, mbali na familia yangu. Hiyo ni hali ya ajabu. Hiyo ni ngumu."

  Mary hakutarajia kufanya urafiki na wageni wake, lakini amefurahishwa na hisia ya jumuiya iliyositawi.

  "Mara nyingi, wakati mwingine hatupati matokeo kutokana na juhudi zetu," anasema. "Lakini kutokana na hizo, ningeweza kuleta mabadiliko katika maisha ya angalau mtu mmoja.”

  Taarifa zilizomo kwenye makala hii zinaweza kuwa zimebadilika tangu zilipochapishwa.

  Vidokezi

  • Katika miezi iliyofuatia uvamizi wa 2022, watu milioni 6 walikimbia Ukrainia wakitafuta usalama

  • Wenyeji walifungua nyumba zao ili kuisaidia Airbnb.org kutimiza ahadi ya kuwapa watu 100,000 makazi ya muda

  Airbnb
  19 Ago 2022
  Ilikuwa na manufaa?