Jinsi unavyoweza kusaidia sehemu za kukaa za dharura wakati wa janga

Pata maelezo kuhusu Airbnb.org na ushiriki kwa kukaribisha wageni au kutoa mchango.
Na Airbnb tarehe 6 Jul 2023
Inachukua dakika 3 kusoma
Imesasishwa tarehe 6 Jul 2023

Wakati majanga ya asili au migogoro mikubwa inapowalazimisha watu kukimbia makazi yao, mojawapo ya mahitaji yao ya dharura ni kupata mahali pa kukaa. Nyumba za muda mfupi huwapa nafasi ya kuzingatia vipaumbele vingine na kufanya mipango ya muda mrefu. Unaweza kuleta tofuati kwa kukaribisha wageni kwenye sehemu za kukaa za dharura au kutoa mchango kwenye Airbnb.org.

Airbnb.org ni nini?

Airbnb.org ni shirika lisilotengeneza faida la Marekani la 501(c)(3) ambalo linafanya kazi bila kutegemea Airbnb. Kazi hiyo ilianza mwaka 2012, wakati Shell, Mwenyeji huko Brooklyn, New York, alipotoa eneo lake bila malipo kwa watu waliohamishwa makazi yako kwa sababu ya Kimbunga cha Sandy. Airbnb iliomba usaidizi kutoka kwa watu wengine katika jumuiya na zaidi ya Wenyeji 1,000 wa eneo husika walifungua nyumba zao kwa watu walioathiriwa na kimbunga hicho.

Ikihamasishwa na vitendo vya Shell, Airbnb ilianzisha mpango ambao uliwezesha Wenyeji kote ulimwenguni kutoa maeneo yao wakati wa shida. Mwaka 2020, mpango huu ukawa shirika lisilotengeneza faida Airbnb.org, lenye dhima na bodi yake ya wakurugenzi.

Leo, Airbnb.org inafanya kazi na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na mashirika ya kibinadamu ulimwenguni kote ili kuunganisha watu kwenye sehemu za kukaa za muda mfupi. Ikifadhiliwa na wafadhili, inatumia majukwaa ya kiteknolojia ya Airbnb na jumuiya ya kimataifa ya Wenyeji ili kukabiliana na majanga ya asili, migogoro na dharura zingine.

Tangu mwaka 2012, Airbnb na Airbnb.org zimewaunganisha karibu watu 300,000 kwenye sehemu za kukaa za dharura, ikiwemo wakimbizi kutoka Ukraine na watu waliohamishwa na matetemeko ya ardhi nchini Uturuki na Siria. Katika miaka mitatu iliyopita, zaidi ya Wenyeji 91,000 katika nchi 189 wamejisajili ili kuwapa wageni makazi. Mahitaji ya msaada yanaendelea kuongezeka.

Ninawezaje kutoa mchango kwa Airbnb.org?

Unaweza kutoa mchango wa mara moja, iwe una sehemu ya kukaribisha wageni au la. Ikiwa unakaribisha wageni mara kwa mara kwenye Airbnb, unaweza kutoa asilimia maalumu ya kila malipo unayopokea. Kwa vyovyote vile, asilimia 100 ya mchango wako inaenda kufadhili sehemu za kukaa za dharura (na si gharama za uendeshaji za Airbnb.org).

Ninawezaje kuwa Mwenyeji wa Airbnb.org?

Ikiwa wewe ni Mwenyeji wa Airbnb, unaweza kutumia tangazo la sasa au kuweka jipya kwa ajili ya nyumba tofauti. Una chaguo la kutoa eneo lako bila malipo au kwa punguzo kupitia Airbnb.org.

Unaweza pia kujisajili ili kukaribisha wageni pekee kupitia Airbnb.org, ambayo inamaanisha utakaribisha wageni tu wanaohitaji sehemu za kukaa za dharura. Ikiwa ni hivi, utakaribisha wageni kwenye sehemu yako bila malipo.

Wageni wa Airbnb.org wanakaa kwao bila malipo. Nafasi zinazowekwa zinafadhiliwa na michango. Kwa kutoa eneo lako bila malipo au kwa punguzo, unaweza kusaidia michango kwenda mbali zaidi na kutoa sehemu za kukaa za dharura kwa watu wengi zaidi.

Airbnb husamehe ada zake zote za huduma kwa ajili ya sehemu za kukaa za Airbnb.org. Nafasi zilizowekwa zinalindwa na AirCover kwa ajili ya Wenyeji.

Wageni wa Airbnb.org ni akina nani?

Wageni wa Airbnb.org mara nyingi wanaalikwa au wanasaidiwa na mashirika yanayojishughulisha na kushughulikia migogoro na makazi mapya ya wakimbizi. Wageni hawawezi kuomba moja kwa moja kupata sehemu ya kukaa ya dharura kupitia Airbnb.org.

Wageni ambao wanastahiki kupata sehemu za kukaa za dharura ni pamoja na:

  • Watu walioathiriwa na majanga makubwa, na wafanyakazi wa misaada wanaoshughulikia majanga hayo kama wafanyakazi rasmi.

  • Wakimbizi, au watu walio katika mchakato wa kutafuta hifadhi, Viza Maalumu ya Wahamiaji, au hali nyingine ya uhamiaji kwa kusudi sawa la kibinadamu.

Wageni wanaostahiki wanaweza kupokea salio la Airbnb.org ili kuweka nafasi ya sehemu ya kukaa ya dharura au mshirika asiyetengeneza faida anaweza kuweka nafasi kwa niaba ya wageni na kusimamia mawasiliano na Mwenyeji.

Sehemu yako inaweza kutoa faraja kwa watu wakati wa shida. Dima, mgeni wa Airbnb.org huko Berlin, aliondoka Ukraine mwaka 2022. Nilikuwa na hisia sana siku hizo za kwanza,” Dima anasema. "Sijui hata ni jambo gani lililokuwa muhimu zaidi kwangu: kuwa katika sehemu salama au kuelewa tu kiasi cha usaidizi ambacho ninapokea."

Je, wageni watajua kwamba mimi ni mchangiaji wa Airbnb.org?

Ndiyo. Kujisajili ili kutoa sehemu za kukaa za dharura bila malipo au kwa punguzo au kuweka michango ya mara kwa mara kutoka kwenye pesa zinazolipwa, kunakupatiabeji ya mchangiaji wa Airbnb.org kwenye wasifu wako wa Mwenyeji.

Mamilioni ya watu ulimwenguni kote wamehamishwa kutoka kwenye nyumba zao kwa sababu ya mgogoro na maafa. Unaweza kuleta tofauti ya kweli katika maisha ya wakimbizi, watu waliohamishwa makwao na wafanyakazi wa misaada kwa kufungua nyumba yako, au kutoa mchango, ili kusaidia sehemu za kukaa za dharura.

Airbnb
6 Jul 2023
Ilikuwa na manufaa?