Nenda mbele ili upate matokeo yaliyopendekezwa

  Jinsi ya kuweka mkakati wa bei

  Bei sahihi inaweza kukusaidia kuwavutia wageni na kuongeza mapato yako.
  Na Airbnb tarehe 1 Des 2020
  Inachukua dakika 3 kusoma
  Imesasishwa tarehe 21 Nov 2022

  Vidokezi

  • Wavutie wageni wako wa kwanza kwa kuweka bei ya kuanzia ambayo ni ya chini kidogo kuliko bei lengwa yako

  • Nyenzo zetu zinaweza kukusaidia kuweka na kurekebisha bei yako, ikiwemo mapunguzo

  Bei ni mojawapo ya vigezo vikuu ambavyo wageni huzingatia wakati wa kuchagua mahali pa kukaa. Haijalishi sehemu yako ni nzuri kiasi gani, ikiwa ina bei ya juu kuliko sehemu zinazofanana nayo zilizo karibu, kuna uwezekano mkubwa wa kukosa kuwekewa nafasi.

  Jaribu kutumia vidokezi hivi ili kujua mkakati wa kupanga bei unaokufaa.

  Fahamu mahali ulipo

  Anza kwa kuangalia bei za wastani. Tafuta matangazo yanayofanana na lako mahali ulipo kwenye Airbnb, kwa kuzingatia:

  • Aina ya nyumba: nyumba, fleti, n.k.
  • Sehemu ambayo wageni watakuwa nayo: nyumba nzima, chumba cha kujitegemea, n.k.
  • Idadi ya wageni wanaoweza kutoshea kwenye eneo lako kwa starehe: idadi ya vitanda na vyumba vya kulala unavyotoa
  • Vistawishi maarufu: Wi-Fi, jiko, wanyama vipenzi wanaruhusiwa, n.k.

  Unapolinganisha bei, chagua tarehe za miezi michache ijayo ili uelewe kikamilifu kilichopo. Nyumba zinazopatikana katika wiki moja au mbili zinazofuata huenda zisiwekewe nafasi kwa sababu zina bei ya juu sana.

  Kutafuta nyakati tofauti za mwaka kunaweza kukusaidia kupata maelezo kuhusu jinsi Wenyeji walio karibu nawe wanavyorekebisha bei yao kulingana na msimu, wikendi na kwa ajili ya hafla maalumu au likizo.

  Toa thamani bora

  Ni muhimu kukumbuka kwamba bei ya kila usiku unayoweka si jumla ya bei ambayo wageni watalipa. Jumla ya bei pia inajumuisha ada zozote za hiari (kwa ajili ya kufanya usafi, wageni wa ziada au wanyama vipenzi) ambazo unaweza kuweka, pamoja na ada ya huduma ya Airbnb.

  Wageni sasa wanaweza kuchagua kuonyesha jumla ya bei mapema katika maeneo ambayo sheria za mahali husika haziihitaji.

  Bei yenye ushindani inaweza kusaidia tangazo lako lionekane na liwe kwenye nafasi ya juu katika matokeo ya utafutaji, ambayo yanaweka kipaumbele kwa jumla ya bei na ubora wa tangazo ikilinganishwa na matangazo yanayofanana nalo mahali hapo. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi matokeo ya utafutaji yanavyofanya kazi.

  Wageni wanaweza kusita kuweka nafasi kwenye tangazo ambalo halina tathmini, kwa hivyo fikiria kuweka bei yako iwe ya chini kidogo kuliko bei uliyokusudia. Mara tu unapokuwa na tathmini nzuri, unaweza kuamua kupandisha bei yako ili ilingane na uhitaji mahali ulipo.

  Baadhi ya gharama unazojumuisha katika bei yako huenda zisiwe wazi kwa wageni. Unatoa vitu vya ziada vya kifahari, kama vile kifungua kinywa kamili, bidhaa za kuoga za kisanii au baadhi ya huduma za kutazama maudhui ya video mtandaoni? Eleza waziwazi katika maelezo ya tangazo lako ili uwasaidie wageni wapate thamani kwenye bei yako.

  Jaribu nyenzo hizi za kupanga bei

  Upangaji bei Kiotomatiki

  Ungependa bei yako ibadilike kiotomatiki kulingana na uhitaji? Washa kipengele cha Upangaji bei Kiotomatiki. Nyenzo hii ya kupanga bei inazingatia zaidi ya sababu 70 tofauti ili kuamua bei bora kwa kila usiku unaopatikana kwenye kalenda yako.

  Bei yako inasasishwa kiotomatiki, kulingana na vitu kama vile:

  • Muda kati ya kuweka nafasi na kuingia: Tarehe ya kuingia inapokaribia
  • Umaarufu wa mahali husika: Idadi ya watu wanaotafuta sehemu za kukaa mahali ulipo
  • Msimu: Mabadiliko ya kimsimu yanayotabirika ya uhitaji wa sehemu za kukaa mahali ulipo
  • Umaarufu wa tangazo: Mara ambazo wageni hutembelea na kuweka nafasi kwenye tangazo lako
  • Historia ya tathmini: Idadi ya tathmini nzuri za wageni unazoandikiwa

  Ili kusaidia kuhakikisha kwamba bei yako inakidhi mahitaji yako, weka bei ya chini na ya juu ya kila usiku kwenye nyenzo ya Upangaji bei Kiotomatiki. Bei yako haitashuka chini ya kiwango hicho isipokuwa uwe unatoa punguzo ambalo pia linatumika. Ikiwa hufurahii bei iliyowekwa na kipengele cha Upangaji bei Kiotomatiki, unaweza tu kuweka nyingine kwa tarehe hiyo kwenye kalenda yako.

  Uhakiki wa bei

  Nyenzo ya kuhakiki bei hukuruhusu kuona bei ya mwisho ambayo wageni watalipa, ikiwemo ada, mapunguzo, promosheni na kodi.

  Ili utumie nyenzo hii, nenda kwenye mipangilio yako ya bei kisha uchague "Hakiki kile ambacho wageni wanalipa." Weka maelezo ya ukaaji, kama vile idadi ya wageni na usiku katika nafasi iliyowekwa na utaonyeshwa mchanganuo wa jumla ya bei ya mgeni na malipo utakayopokea.

  Mapunguzo

  Fikiria kutoa mapunguzo kwenye ukaaji wa muda mrefu ili kuwavutia wageni waweke nafasi. Mapunguzo ya kila wiki na kila mwezi yanaweza kusababisha nyumba yako ipate idadi kubwa ya ukaaji, idadi ndogo ya wageni wanaotoka na wengine kuingia na wewe kuwa na kazi kidogo.

  Inaweza kuchukua muda kabla ya mkakati wako wa bei kuwa sahihi. Kwa sasa, endelea kuwa mwepesi kubadilika na uzingatie kuwaridhisha wageni. Tathmini nzuri zaidi zinaweza kusaidia kukuza biashara yako ya kukaribisha wageni.

  Taarifa zilizomo kwenye makala hii zinaweza kuwa zimebadilika tangu zilipochapishwa.

  Vidokezi

  • Wavutie wageni wako wa kwanza kwa kuweka bei ya kuanzia ambayo ni ya chini kidogo kuliko bei lengwa yako

  • Nyenzo zetu zinaweza kukusaidia kuweka na kurekebisha bei yako, ikiwemo mapunguzo

  Airbnb
  1 Des 2020
  Ilikuwa na manufaa?